Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeeleza katika taarifa yake: "kwa mujibu wa sheria za Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio anawanyima na kuwabatilishia viza wanachama wa Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) na Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA) kabla ya Mkutano Mkuu ujao wa Umoja wa Mataifa".
Taarifa hiyo imebainisha kuwa Ujumbe wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina katika Umoja wa Mataifa utapewa msamaha wa marufuku hiyo kulingana na Mkataba wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Katika kutetea hatua yake hiyo, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imezituhumu PLO na PA kuwa zimeshindwa kuukana ugaidi, kuchochea utumiaji nguvu, na kuendeleza "kampeni za sheria za kimataifa" kupitia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).
Katika taarifa tofauti alizotoa kupitia mtandao wa kijamii wa X, naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tommy Pigott amesema: "kabla hatujawachukulia kwa uzito kuwa ni washirika katika amani, PA na PLO lazima ziukane kikamilifu ugaidi na ziache kufuatilia kwa upande mmoja na bila tija kutambuliwa nchi dhahania (ya Palestina)."
Haijabainika mara moja kama Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas ataweza kuhudhuria Mkutano Mkuu wa UN na kutoa hotuba yake ya kawaida ya kila mwaka katika mkutano huo.
Mnamo Julai 31, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilikiwekea vikwazo Chama chah Ukombozi wa Palestina, PLO na Mamlaka ya Ndani ya Palestina PA, na kuwanyima wanachama wao viza za kuingilia nchini humo. Lakini mkabala wake, hivi majuzi Washington iliwaondolea vikwazo kwa walowezi wa kizayuni wa Israel wanaoshutumiwa kwa kufanya mashambulizi na hujuma dhidi ya Wapalestina.
Hatua hiyo ya Marekani ya kufuta viza za maafisa wa Palestina imechukuliwa wakati Ufaransa, Uingereza, Canada na Australia zimetangaza mipango ya kulitambua taifa la Palestina katika mkutano ujao wa UNGA, na kuungana na nchi 147 ambazo tayari zimeshafanya hivyo.../
Your Comment